Back

ⓘ Homo
Homo
                                     

ⓘ Homo

Homo ni jenasi ambayo katika uainishaji wa kisayansi inajumlisha binadamu na spishi zilizokoma zilizofanana naye sana. Wanasayansi wamependekeza zaidi ya spishi 12 za jenasi Homo.

Jina Homo ni la Kilatini, likiwa na maana ya "mtu", na kwa asili linahusiana na neno humus, "ardhi".

                                     

1. Historia ya awali

Jenasi hiyo inakadiriwa kuanza kuwepo miaka milioni 2.1 - 2.8 iliyopita kutokana na spishi mojawapo ya nusukabila Australopithecina siku hizi linatumika pia jina Hominina iliyokuwepo kuanzia miaka milioni 5.6 hadi 1.2 iliyopita.

Spishi ya kwanza ya jenasi hiyo inawezekana ilikuwa ile ya Homo habilis, yaani mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vifaa. Mabaki yake yalipatikana huko Oltupai Tanzania. Huyo anafikiriwa kutokana na Australopithecus garhi ambaye kabla yake alikuwa ameanza kutengeneza vifaa kwa mawe.

Hata hivyo mnamo Mei 2010 huko Afrika Kusini yalipatikana mabaki ya Homo gautengensis, spishi inayofikiriwa na wengine kuwa ya kale kuliko Homo habilis, lakini wengine wanaijumlisha katika jina Homo abilis. Tena wataalamu wengine wanaona spishi hizo mbili hazistahili kuitwa Homo, ila Australopithecus.

Kutokana na Homo habilis au Australopithecus habilis alipatikana miaka milioni 2 iliyopita Homo erectus aliyekuwa wa kwanza kusimama daima juu ya miguu yake miwili, kuwinda na kumudu moto, na ambaye alienea kote Asia na Ulaya aliyebaki Afrika anaitwa pia Homo ergaster kabla ya kugawanyika katika nususpishi au spishi mpya mbalimbali kama Homo georgicus, Homo antecessor, Homo heidelbergensis, wa kwanza kujenga makazi ya kudumu na kuzika wafu, n.k. Kwa jumla Homo erectus alidumu zaidi ya miaka milioni moja. Wengi wanaona spishi nyingi zilizopendekezwa kuwa nususpishi tu za Homo erectus.

Miaka 800.000–200.000 iliyopita, wakati wa mabadiliko makubwa ya hali ya hewa, ubongo wa jenasi hiyo ulikua sana na kupata uwezo wa kufanya mambo mengi mapya katika mahusiano na katika kukabili mazingira ambayo yalizidi kubadilika na kudai maitikio tofauti ili kudumisha uhai wa jenasi yenyewe.

Kufikia miaka 100.000 au 50.000 hivi iliyopita, spishi zote za jenasi Homo zilikuwa zimekoma, isipokuwa Homo sapiens aliyekuwa ametokana na Homo heidelbergensis miaka 300.000 hivi iliyopita.

Baadhi ya wataalamu wanahesabu Homo neanderthalensis na mtu wa Denisova kama nususpishi za Homo sapiens zilizoweza kuzaliana na watu wa kisasa waliotokea Afrika.

Spishi zote za jenasi Homo zimekoma, isipokuwa Homo sapiens binadamu.