Back

ⓘ Upendo
Upendo
                                     

ⓘ Upendo

Upendo ni neno linalotumika kwa maana mbalimbali kuanzia hali ya nafsi ya binadamu hadi kwa Mungu. Linatokana na kitenzi "kupenda" na kufanana na pendo, mapendo, mapenzi, n.k.

Hapa linatumika kwa maana ya juu zaidi kulingana na Kigiriki "agape" na Kilatini "caritas".

                                     

1. Katika Ukristo

Kufuatana na Maandiko Matakatifu, hasa ya Mtume Paulo, katika teolojia ya Ukristo ni mojawapo kati ya maadili ya Kimungu, pamoja na imani na tumaini.

Kadiri ya dini hiyo, inatupasa tumpende Mungu pekee, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, kadiri tunavyoweza, kwa kuwa ndiye asili ya uhai wetu na ya wema wote." Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote” Kumb 6:4." Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu” Mk 10:18.

Halafu tupende viumbe vya Mungu pia kadiri anavyotaka tuwapende kwa kuwa mwenyewe anawapenda." Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba” Hek 11:24." Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Mtu akisema, Nampenda Mungu’, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona. Na amri hii tumepewa na yeye: ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake” 1Yoh 4:11.20-21.

Kielelezo cha upendo ni Yesu Kristo, aliyefikia hatua ya kujitoa kafara kwa ajili yetu na kutuombea sisi wakosefu tuliomtesa." Ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi” Rom 5:7-8." Nimewapa kielelezo; ili kama mimi nilivyowatendea, nanyi mtende vivyo” Yoh 13:15." Muenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yenu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato” Ef 5:2." Katika hili tumelifahamu pendo: kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu” 1Yoh 3:16.

Lakini tusimfuate Yesu kama kielelezo tu, bali tuishi ndani yake na kwa ajili yake, kwa kuwa ndiye uhai wetu." Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu, kadhalika nabyi, msipokaa ndani yangu” Yoh 15:4." Alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao” 2Kor 5:15." Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu” Kol 3:3-4.

Kadiri ya madhehebu kadhaa, tunaweza kufuata mfano wa watu wengine kadiri walivyomfuata Yesu. Ndio wale tunaowaita watakatifu, kwa kuwa Kanisa limewaweka mbele yetu kama kielelezo wazi cha upendo kamili." Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate” 2Thes 3:9." Mnifuate mimi kama mimi ninavyomfuata Kristo” 1Kor 11:1." Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi. Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo” Fil 3:17; 4:9.

Upendo wa Mungu si hisia ya moyo, inayoweza kubadilikabadilika, bali ni msimamo wa dhati unaojitokeza katika matendo." Lakini mtu akiwa na riziki ya dunia, kisha akamwona ndugu yake ni mhitaji, akamzuilia huruma zake, je, upendo wa Mungu wakaaje ndani yake huyo? Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli” 1Yoh 3:17-18.

Basi, huo upendo ambao tumpende Mungu na viumbe vyake si pendo la kibinadamu tu, bali ni uleule ambao mwenyewe anajipenda, anatupenda na kutushirikisha, yaani ni Roho Mtakatifu." Pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi” Rom 5:5." Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza” 1Yoh 4:7.16.19.

Tunaweza kuwa na kiasi chochote cha upendo huo wa Kimungu, lakini tuwe daima tayari kuupokea upya na kuutekeleza uzidi kustawi bila mwisho." Bwana na awaongeze na kuwazidisha katika upendo, ninyi kwa ninyi, na kwa watu wote” 1Thes 3:12." Pendo lenu lizidi kuwa jingi sana” Fil 1:9.

Upendo unatakiwa kustawi zaidi na zaidi bila mwisho, kwa kuwa ndio mfumo wake. Upendo wa kweli haufuati kipimo: kiasi cha kupenda ni kupenda bila kiasi." Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma” Lk 6:36." Kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu, hali akijua ya kuwa saa yake imefika, atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwengu, aliwapenda upeo” Yoh 13:1.

Upendo utakamilika mbinguni, ambapo tutamuona Mungu alivyo na kuvutiwa naye tusiweze kubandukana naye milele." Upendo haupungui neno wakati wowote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika. Maana wakati wa sasa tunaona kwa kioo kwa jinsi ya fumbo; wakati ule tutaona uso kwa uso; wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana” 1Kor 13:8.12." Na uzima wa milele ndio huu: wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma” Yoh 17:3.

Hivyo Ukristo unatuelekeza kuona maisha haya kama safari ya kulenga upendo kamili, ambapo Roho Mtakatifu anatunasukuma tusonge mbele kwa hatua za upendo mkubwa zaidi na zaidi." Nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu, katika Kristo Yesu. Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lolote, Mungu atawafunulia hilo nalo. Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo” Fil 3:13-16.

Utekelezaji wa upendo unadai uendane na maadili mengine yote, la sivyo si wenyewe; sanasana ni pendo la kibinadamu tu lisilopatana na Mungu." Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote; hutumaini yote, hustahimili yote” 1Kor 13:4-7." Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu” Math 6:2.

Maadili mengine yasipoendana na upendo, huwa yamekufa, kwa kuwa upendo ndio uhai wa hayo yote." Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je, ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba’, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake” Yak 2:14-17." Nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu” 1Kor 13:3.

Maadili yanayoendana na upendo ni hasa imani na tumaini." Hatuachi kuikumbuka kazi yenu ya imani, na taabu yenu ya upendo, na saburi yenu ya tumaini lililo katika Bwana wetu Yesu Kristo, mbele za Mungu Baba yetu” 1Thes 1:3." Sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu” 1Thes 5:8." Sikuzote tukiwaombea, tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote, kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni” Kol 1:3-5." Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo” 1Kor 13:13.

Hayo matatu yanaitwa maadili ya Kimungu kwa kuwa asili na lengo lake ni Mungu mwenyewe. Hatuwezi kujipatia hayo, bali tunamiminiwa naye kwa pamoja tuweze kumsadiki, kumtumaini na kumpenda inavyotupasa tuwe marafiki wake." Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu” Ef 2:8." Ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana” 1Thes 4:9.

Pamoja na imani na tumaini, upendo unadai maadili ya kiutu, ambayo yote yanategemea manne ya msingi: busara, haki, nguvu na kiasi." Huwafundisha watu kiasi, na ufahamu, na haki, na ushujaa; wala hakuna mambo ya kuwafaa zaidi kwa maisha” Hek 8:7.