Back

ⓘ Elenzian J. Komba
                                     

ⓘ Elenzian J. Komba

Elenzian JK ni Mwandishi chipukizi na hodari anayekuja kwa kasi kubwa kwenye uga wa Ushairi wa Kiswahili. Anatambulika kwa lakabu ya Kishairi ya "Kalamu Ndogo" ambayo yeye hujisikia fahari sana kujitambulisha kwayo, na pengine hii ndiyo sababu iliyopelekea nomino ya diwani yake ya kwanza iliyochapwa mwaka 2019 kujulikana kama WINO WA KALAMU NDOGO

Mbali na jina la Kalamu Ndogo, wengine hupenda pia kumuita Mwanasayansi Mshairi kutokana na ukweli kwamba kitaaluma yeye ni Mwanafunzi wa masomo ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM

KUZALIWA. Bwana Elenzian JK ama Kalamu Ndogo kwa jina la kishairi, alizaliwa tarehe 11 ya Mwezi Aprili, mwaka 1996 mkoani Dar er salaam, nchini Tanzania

Alianza elimu ya msingi mwaka 2003 katika shule ya Msingi Mtambani, baadaye alihamia shule ya Msingi Majohe iliyopo pembezoni kidogo mwa mkoa wa Dar es salaam, ambapo ndipo alipomalizia elimu yake ya msingi mwaka 2009.

Mwaka 2010 alianza elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Nguvu Mpya iliyopo Kata ya Chanika Dar es salaam, na kuhitimu mwaka 2013. Akiwa shuleni hapo ndipo alitambua kipawa chake cha uandishi na Ushairi kupitia msaada wa Rafiki zake na Walimu wake shuleni hapo.

Mwaka 2014 alijiunga na shule ya sekondari ya ufundi Ifunda huko Iringa kwa ajili ya elimu ya kidato cha tano na cha sita katika tahasusi ya PCB na kuhitimu mwaka 2016. Pia akiwa shuleni hapo ndipo alianza kuuvalia njuga Ushairi kwa kushiriki mashindano madogomadogo na kuhifadhi tungo zake kimaandishi. Zaidi ya 30% ya tungo zilizounda diwani yake ya kwanza ya Wino wa Kalamu Ndogo alizitunga wakati huo.

Mwishoni mwa mwaka huo wa 2016 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu, akisomea Shahada ya Elimu katika Sayansi na TEHAMA BEd Sc. ICT ambapo mwaka 2019 ni mwaka wake wa mwisho kimasomo.

Ushairi, kama ukweli wenyewe ulivyo, ni sanaa ya lugha ambayo imeonekana kufifia kidogo kwa miaka ya hivi karibuni, hii inathibitika kupitia, kupungungua kwa vyombo vya habari vinavyopeperusha bendera ya sanaa hii ya ushairihii pia inaweza kutajwa kama mojawapo ya sababu za ufifiaji wake. Uthibitisho mwingine ni kupitia kupungua kwa idadi ya wasomaji wapenzi, lakini pia kupitia kupungua kwa idadi ya waandishi wanaothubutu kutunga na kuiandikia aina hii ya maandishi ya kubuni ambayo ni kongwe na tajiri. Pamoja na kufifia huko ama pengine ufifishwaji huo, bado wapo wadau na watunzi mbalimbali wanaoibuka kila uchwao, na kulipigia mbizi enoeo hili, ili kujaribu kulihuisha kama sehemu ya jitihada za urithishwaji wa sanaa hii ya Kiafrika ambayo ni mbavu za utamaduni wetu. bwana Elenzian JK ni mmojawapo kati ya wadau na Watunzi hao wenye ari na hamasa ya kuuinua ushairi kama fani yenye nguvu kubwa katika kuburudisha na kufikisha ujumbe kwa jamii.

Mbali na kufanikiwa kuchapa kitabu chake hicho cha kwanza, Kalamu Ndogo, kwa muda mrefu amekuwa akitunga tungo na kusomwa kwenye matukio kadha wa kadha ya kijamii, pia amekuwa akichapa tungo zake kupitia mitandao ya kijamii kama WhatsApp, Facebook Elenzian Komba na Instagram Elenzian_jk ambayo kupitia hiyo idadi ya wasomaji wake imekua ikiongezeka siku baada ya siku, pia mara kadhaa amekua akishiriki mashindano ya utunzi na uandishi, kama njia moja wapo ya kufikisha ujumbe na kuukuza uandishi wake kama Mtunzi anayechipukia.