Back

ⓘ Malipo
Malipo
                                     

ⓘ Malipo

Malipo ni pesa au kitu atoacho mtu kulipia kitu alichonunua au kazi au huduma aliyofanyiwa. Malipo pia yanaweza kuwa ya shukrani kwa mazuri aliyofanyiwa mtu

                                     

1. Msamiati wa malipo mbalimbali

 • Kodi - mapato au malipo kwa serikali kutokana na mishahara ya wafanyakazi au mapato mengine.
 • Tapisho - malipo kwa ngariba kwa ajili ya utahirishaji.
 • Kiinuamgongo/Pensheni/Bonasi - malipo baada ya kustaafu.
 • Kipkasa/Kipamkono/Jazua/Ukonavi - malipo anayopewa biharusi aonwapo mara ya kwanza.
 • Dhamana - malipo kwa niaba ya mtu ili ahudumiwe au aachiliwe huru kwa muda maalumu kesi au daawa inpoendelea mahakamani.
 • Masurufu - pesa za matumizi ya safarini, matumizi ya nyumbani, njiani au mfukoni pocket money.
 • Rada - malipo yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu kurudi mtu aliyefanya jambo ovu.
 • Karo - malipo ya masomo shuleni.
 • Mchango - malipo ya hiari kwa ajili ya kujenga au kutoa hisani au msaada kwa yule anayehitaji.
 • Faini - malipo anayotozwa mhalifu mahakamani.
 • Nauli - malipo ya kusafiria.
 • Utotole/Kiangazamacho/Machorombozi/Chorombozi Kiokozi - zawadi ya ugunduzi wa kitu au kushuhudia jambo linapofanyika mahali wakati fuluani.
 • Faida/Natija/Tija - pesa za ziada azipatazo mfanyabiashara.
 • Koto/Ufito - ada anayotoa mzazi kwa mwalimu anapomwingiza mtoto wake chuoni.
 • Mbiru - malipo kwa serikali kutokana na mishahara ya wafanyakazi wake.
 • Arshi / Dia - malipo kwa ajili ya kumtoa mtu damu.
 • Kivusho - malipo ya kuvuka daraja, mto au kivuko chochote.
 • Fungule/Kanda - malipo ya kwanza kwa mganga.
 • Rehani - malipo ya kitu kilichowekwa dhamana ili kukombolewa baadaye.
 • Rushwa/Kadhongo/Chirimiri/Chauchau/Kilemba/Mvugulio - malipo au zawadi anayotoa mtu ili kupata haki asiyostahili.
 • Ujira - malipo ya kazi yoyote ya mkono.
 • Arbuni/Rubuni/Advansi/Chambele/Kishanzu - malipo ya kwanza ya kuzuia kitu kisiuzwe.
 • Fola - malipo ya kumshika mtoto mchanga kwa mara ya kwanza.
 • Karisaji - malipo ya pesa ya muda uliopita.
 • Kombozi - malipo ya kukombolea kitu au mtu.
 • Kikunjajamvi - ada idaiwayo kwa wafanyabiashara au wakazi wa mabaraza ya kiasili na ya kizamani ambayo hujumuisha fedha au mali, kwa mfano: kondoo, mbuzi, kuku n.k.
 • Kiingilio - malipo ya kuingia mahali kwa mfano mchezoni au densi.
 • Karadha - mkopo bila riba au malipo ambayo ni sehemu ya mshahara apewayo mtu katikati ya mwezi.
 • Thawabu - malipo anayopata mtu kutoka kwa Mwenyezi Mungu ajili ya kutii amri zake.
 • Mtaji - pesa za kuanzishia biashara.
 • Mrabaha - faida au pato linalotokana na biashara; pia malipo anayopewa mwandishi au msanii na kampuni iliyotoa kazi yake kila baada ya kipindi fulani cha mauzo.
 • Ushuru - malipo yanayotozwa bidhaa forodhani.
 • Fichuo - malipo anayopewa kijana anapotoka jandoni.
 • Haka - malipo ya kufidia kosa fulani katika mambo ya familia.
 • Bakora - zawadi ambayo baba humpa fundi akitaka mwanawe afundishwe ufundi.
 • Riba - faida inayotozwwa na mkopeshaji au ziada ya benkini.
 • Marupurupu/Posho - malipo anayopata mtu zaidi ya malipo yake ya kawaida.
 • Ridhaa - malipo apewayo mtu aliyevunjiwa hadhi au heshima yake.
 • Mwago - malipo kwa mke wa kwanza mume anapooa mke wa pili.
 • Pango - kodi ya nyumba alipwayo mwenye nyumba baada ya kipindi fulani kulingana na makubaliano.
 • Kibarua - malipo ya kufanya kazi kutwa au malipo ya usiku.
 • Mshahara - malipo ya mfanyakazi mwishoni mwa kila mwezi.
 • Mapoza - malipo unayomlipa uliyemwudhi ili kuondoa hasira zake.
 • Mukafaa - malipo ya mshahara kwa mfanyakazi kutokana na faida iliyopatikana.
 • Kudu - malipo alipayo mwari kwa nyakanga kama adhabu kwa kukosa adabu alipokuwa unyagoni.
 • Fidia - malipo yalipwayo na shirika la bima kwa ajili ya hasara au maumivu yaliyompata mtu.
 • Mahari - malipo ya kuoa ua kuolewa.
 • Kilemba - ada ya harusi wanayopewa wajomba wa bibiharusi; pia malipo anayotoa mwanagenzi kwa mhunzi wake baada ya kuhitimu mafunzo yake.
 • Zaka - moja ya kumi ya mapato ambayo waumini wa dini humtolea Mwenyezi Mungu kama shukrani.
 • Risimu - bei ya kwanza ya kukinunua kitu mnadani.
 • Advansi /Karadha - malipo yanayotolewa kabla ya wakati wake kuwadia au kazi kumalizika.
 • Zawadi/Tuzo/Takrima/Hidaya - atunukiwacho mtu kama ni ishara ya mapenzi, wema, ushindi au kwa utendaji mzuri wa shughuli.
 • Bahashishi - malipo ya kuonesha shukrani.
 • Honoraria - malipo apewayo mtu kama bahashishi kwa kazi maalumu aliyoifanya.
 • Urithi/Urathi - malipo anayopewa mtu kutokana na mali ya marehemu.